VIONGOZI WA PAROKIA

VIONGOZI WA PAROKIA

Wednesday, 30 March 2016

BABA MTAKATIFU FRANCISKO AYASEMA HAYA JUU YA HURUMA KUU YA MUNGU

Huruma ya Mungu: Ina samehe; inasafisha na kupyaisha maisha!

Ee Mungu, unirehemu, sawa sawa na fadhili zako; kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu; unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu. Kwa sala hii ya Zaburi, Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 30 Machi 2016 amehitimisha Katekesi kuhusu huruma ya Mungu kadiri ya Agano la Kale kwa kufanya tafakari ya Zaburi ya 51, Unihurumie Ee Mungu “Miserere”, sala ya mwamini anayetubu na kuomba huruma na msamaha wa Mungu, huku akiachia upendo wa Mungu uweze kuisafisha roho yake. Katekesi hizi ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

 Baba Mtakatifu anasema, Zaburi ya 51 kadiri ya Mapokeo ni sala ya toba kutoka kwa Mfalme Daudi, baada ya kutenda dhambi kule Bathsheba. Hii ni sala ya Zaburi inayokimbilia huruma na wema wa Mungu; kwa mwamini kutambua dhambi zake, tayari kuzitubu na kuziungama, huku akiwa na matumaini kwa Mungu mwingi wa rehema anayesamahe na kusahau.Mzaburi anamwomba Mungu ili aweze kuyafuta kabisa makosa yake na kumsamehe dhambi zake, Mzaburi anaimba utenzi wa sifa kwa haki na utakatifu wa Mungu usiokuwa na mipaka. Anamwomba Mwenyezi Mungu kumwosha kabisa na uovu wake na hatimaye, aweze kumuumbia moyo safi na kuifanya roho iliyotulia ndani mwake, ili aweze kuwafundisha wakosaji njia zake na wenye dhambi kurejea kwa Mungu. Msamaha wa Mungu ni kielelezo cha juu kabisa cha huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Bikira Maria ili awawezeshe kuwa mashuhuda wenye mvuto na mashiko wa huruma ya Mungu inayosamahe dhambi za binadamu, kiasi hata cha kuwaumbia moyo mpya, ili hatimaye kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu unaowapatanisha walimwengu!

Baba Mtakatifu amewatakia wote huruma ya Mungu katika maisha yao.Waamini wote wanahitaji kuonjeshwa huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku! Katika kipindi hiki cha Pasaka, waamini wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka na kuendelea kumshukuru kwa kuwakirimia huruma na msamaha usiokuwa na kifani; msamaha unaosafisha na kuleta mabadiliko katika maisha. Waamini kwa kusamehewa dhambi zao, wanakuwa kweli ni viumbe wapya katika Kristo Yesu!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni changamoto kwa waamini kutambua kwamba, wanahitaji huruma ya Mungu katika maisha yao; ili kuwawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili huruma, furaha na imani.Yesu Mfufuka katika kipindi hiki cha Pasaka aendelee kuwaimarisha waja wake katika imani, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda amini wa huruma na upendo wake kwa jirani zao; waendelee kuwa ni mashuhuda wa ahadi za Ubatizo!

PICHA: TAZAMA PICHA 10 ZA IGIZO LA MATESO YA YESU KRISTO [VIWAWA-UBUNGO PARISH]

igizo la mateso ya yesu kristo katika parokia ya ubungo msewe siku ya ijumaa kuu.